KUMBUKUMBU YA JUBILII YA MIAKA 50 YA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA DAYOSISI YA PARE
UTANGULIZI
Kijiografia eneo la Pare (Vuasu) liko Kaskazini mwa Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro, kwa wakati huo ilijulikana kama Wilaya ya Pare iliyojumuisha eneo la Same na Mwanga. Eneo la Vuasu lipo kwenye maeneo ya milimani na tambarare kuanzia Kilevo upande wa kaskazini hadi Bendera upande wa kusini na upana wake kutoka mto Pangani upande wa magharibi mpaka mbuga ya Mkomazi upande wa mashariki.
Eneo la Milima lina vilele virefu ambavyo ni Shengena (kilele kirefu kuliko vyote) kilichoko upande wa kusini (Same), na Kamwala upande wa kaskazini (Mwanga). Eneo hili lina makabila makubwa matatu ambayo ni Vaasu walioenea kutoka kaskazini mpaka kusini wakiwa na lugha yao ya Chasu, Wagweno katika eneo la kaskazini wakizungumza Kigweno na Wamasai katika baadhi ya maeneo ya tambarare wakizungumza Kimasai; pia wako wahamiaji wachache ambao baadhi yao ni Wachaga, Wasambaa na wengine kwa uchache. Hata hivyo lugha ya Chasu inaeleweka zaidi katika makabila yote ya eneo hili.
Hapo mwanzoni kabla ya kuingia Injili, eneo hili lilikuwa na utamaduni wake, watu wake wakivaa ngozi za wanyama na kuishi katika vibanda vidogo, na njia nyembamba zinazopitia vichakani, watu waliishi kwa hofu ya kukutana na watu wengine wasiowajua, kulikuwa na vita vya mara kwa mara vilivyohusisha kunyang’anywa mali zao hasa mifugo.
Baadhi ya mila na tamaduni zilileta madhara makubwa katika jamii iliyokuwepo mfano watoto waliozaliwa wakiwa na ulemavu wa aina yoyote na ambao katika ukuaji walitangulia kuota meno ya juu, waliuawa kwa kufikiri na kuamini kuwa ni mkosi. Ujio wa Wamisionari ulibadilisha mtazamo na kuondoa hofu mbalimbali zilizoifunga jamii iliyokuwepo. Injili ikaenezwa na Wamisionari wakisaidiana na vijana waliokuwa wa kwanza katika kuamini Ukristo. Mabadiliko yakaanza kuonekana kama itakavyoelezwa kwenye Historia hii.
HISTORIA YA KUENEA KWA INJILI ENEO LA VUASU
Kuenea kwa Injili katika eneo la Vuasu ni matokeo ya kazi kubwa ya kuhubiri Injili iliyofanywa na Wamisionari wa Kilutheri waliotumwa na Chama cha Missioni cha Leipzig ambao walianzisha kituo chao cha kwanza kule Nkwarungo Machame (Moshi) mwaka 1893. Kutokea hapo wamisionari hawa walienea hadi eneo la milima ya Vuasu inayokaliwa na Vaasu. Kuanzia kipindi hicho kazi ya kukagua eneo hili ilifanywa na Wamisionari tofauti. Tarehe 10/07/1900 Mchungaji aliyeitwa Hans Fuchs alifika na kukaa Shighatini akiwa na umri wa miaka 22. Mchungaji huyu alifanikiwa kueneza Injili katika eneo hili kwa sababu alitumia lugha ya Chasu kuwasiliana na wenyeji. Mnamo tarehe 07/08/1904 kukawa na Ibada ya ubatizo wa kwanza wa kihistoria wa vijana watano. Vijana hao ni Kilevo Kisaka aliyeitwa Benjamini, Lukwaro Kilenga aliyeitwa Yohana, Msisiri Kijo aliyeitwa Manase, Kisamu aliyeitwa Yosefu, Dundure Msechu aliyeitwa Andrea. Kutokea hapo Injili ikaenea maeneo mengine mengi ya Vuasu.
Tarehe 19/02/1904 Mchungaji aliyeitwa Paul Rother akaanzisha missioni ya Bombo (Gonja)
Tarehe 08/02/1908, Mchungaji aliyeitwa Jacob Dannholz akaanzisha missioni ya Mbaga.
Januari 1909 Mchungaji aliyeitwa Ludwig Oldewage akaanzisha missioni ya Vudee.
Octoba 1913 Mchungaji aliyeitwa Otto Hauptmann akaanzisha missioni ya Usangi.
Hivyo vijana wengi wakabatizwa na kufundishwa kusoma na kuandika, na kupewa wajibu mbalimbali katika Kanisa.
Mwaka 1914 vita kuu ya kwanza ya dunia ilianza na kumalizika mwaka 1918 hivyo kuvuruga kazi ya Injili katika eneo hili kama ilivyokuwa katika maeneo mengi ya Tanganyika. Wamisionari wengi walikamatwa na kupelekwa gereza la Tanga na hatimaye kuhamishiwa Kairo Misri. Wakati wa vita kuu ya kwanza ya dunia kazi ya Elimu na Injili katika eneo la Vuasu iliendelezwa na walimu na wainjilisti wazawa. Andrea Msechu misioni ya Shighatini, Abrahamu Itunda misioni ya Bombo, Martini Shafuri misioni ya Mbaga, Tuvana Mnavu Msolo misioni ya Vudee na Nathanaeli Mgaya misioni ya Usangi. Vituo vingi vya Wamisionari vilitikiswa na vita hii. Baada ya vita kuu ya kwanza Wamisionari wengi walilazimika kuondoka na kurudi Ujerumani hivyo uongozi wa Kanisa kubaki mikononi mwa wenyeji.
Mwaka 1930 Mchungaji Hans Fuchs alibatiza watu wazima 134 huko Shighatini, Mchungaji Michaeli akabatiza watu wazima 56 huko Vudee na watu wazima 61 huko Mbaga; vile vile Mchungaji Guth alibatizwa watu wazima 64 huko Bombokati ya mwaka 1931 na 1932.
Tarehe 27/04/1934 sehemu zote za Vuasu na Kilimanjaro yote zilipatwa na msiba wa kufiwa na Mmisionari hodari wa kwanza Mchungaji Hans Fuchs aliyefariki ghafla akiwa safarini kikazi kule Mwika, mwili wake ulibebwa kurudishwa kwenye Kituo chake cha kazi, na tarehe 28/04/1934 akazikwa huko Shighatini. Katika mwaka huo 1934 mwezi wa tano Walimu wenyeji 4 walibarikiwa kuwa Wachungaji katika missioni za eneo la Vuasu na kupewa wajibu wa kuongoza maeneo hayo kama ifuatavyo; Mchungaji Abrahamu Itunda akapewa kuisimamia missioni ya Bombo, Mchungaji Zakayo Msumba akapewa kuisimamia missioni ya Vudee, Mchungaji Nathanaeli Mgaya akapewa kuisimamia missioni ya Usangi, Mchungaji Andrea Msechu akapewa kuisimamia missioni ya Shighatini. Martini Shafuri alisubirishwa mwaka mmoja na kubarikiwa kuwa Mchungaji mwaka 1935 akapewa kutunza misioni ya Mbaga.
Pamoja na hayo katika maandalizi ya vita kuu ya pili ya dunia mwaka 1935 Adolf Hitler aliagiza misaada yote iliyokuwa inaletwa Afrika isimamishwe ili isiathiri maandalizi ya vita, hivyo kazi ya Injili ikaathirika katika maeneo mengi likiwepo eneo la Vuasu. Pamoja na athari hizo wachungaji wenyeji na Wamisionari wachache waliobaki waliendeleza Injili, hivyo kazi ya Mungu haikusimama.
Mwaka 1940 Wamisionari waliondolewa wakati eneo la vuasu likiwa na wakristo watu wazima 3,058 na watoto 3,289. Tayari misioni katika eneo la Vuasu zilikuwa zimefungua vituo kwenye maeneo yake:
Misioni ya Shighatini vituo vya; Msangeni, Kifula, Mruma, Kilevo, Kiruru, Ndambwe, Mcheni, na Kitoghoto.
Misioni ya Bombo vituo vya; Mtii, Maore, Mramba, Ntenga, Mvango, Ivuga, Makasa, Kihurio na Ndungu.
Misioni ya Mbaga vituo vya; Msindo, Marindi, Madiveni, Kisiwani na Same.
Misioni ya Vudee vituo vya; Chome, Kwanamburi, Mhezi, Mhero, Mtwana, Mwembe, Makanya, Chambogho, Duma, Ndolwa, Mkanyeni na Dangaseta
Misioni ya Usangi vituo vya; Kwamsembea, Mchali, Kivindu, Ndanda, Makandeni (Ndorwe), Toloha na Kisangara Juu.
Changamoto zilizojitokeza wakati huo ni kwamba walimu walioajiriwa na Kanisa waliacha kazi ili wakaajiriwe na serikali ambapo walipewa mishahara mizuri. Lakini pia kukawa na ushindani mkubwa wa dini na madhehebu mengine.
Mwaka 1943 wenyeji wawili Zefania Mtango (Bombo) na Simeoni Mbatiani (Shighatini) walihitimu mafunzo ya uchungaji chuoni Machame na kubarikiwa kuwa wachungaji. Pia katika mwaka huo ndipo Kanisa la Kilutheri Tanganyika ya Kaskazini lilipoanzishwa na mfumo wa kuita makanisa sharika ulianza.
Mnamo mwaka 1945 vita kuu ya pili ilipomalizika hali ya Amani, Furaha na Utulivu vilirejea na ari ya kufanya kazi ya Mungu ikashamiri. Kuanzia mwaka 1941 mpaka 1958 sharika za Mtii, Ivuga, Same na Mruma ziliongezeka, na shule za kati za Kifula, Shighatini, Dindimo (Bomo), Manka (Mbaga) na Vudee zilijengwa.
Mwaka 1950 wanafunzi sita kutoka eneo la Pare walifuzu masomo yao katika chuo cha uchungaji Lwandai. Wanafunzi waliomalizia masomo yao Lwandai ni: Eliewaha Mshana (Usangi), Yonazi Kikuji (Bombo) akitokea Ntenga, Sila Msangi ((Kifula), Danieli Kimbwereza (Mbaga), Elinisafi Mapunjo (Vudee) akitokea Chome na Elirehema Mwanga (Shighatini). Baadhi ya wachungaji hawa walishika nafasi muhimu sana katika Kanisa na katika jamii: Eliewaha Mshana akawa mwafrika wa kwanza kuwa mkuu wa chuo cha Uchungaji Makumira, baadae akachaguliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Pare; Elirehema Mwanga akawa mzawa wa kwanza kuwa mkuu wa chuo cha Biblia Mwika pia akawa Rais kipindi cha mpito cha Kanisa la Usambara Digo. Sila Msangi akiwa mtunzi wa nyimbo za Kikristo zilizotumika mahali pengi ndani na nje ya Tanganyika. Mwaka 1950 walimu wa kike waliongeza hamasa mashuleni. Wakati huu Mchungaji Andrea Msechu aliandika kitabu cha “Mburi ja Biblia”.
Mwaka 1954 shule za kati (Middle Schools) tano za Kifula, Shighatini, Dindimo (Bombo), Manka (Mbaga) na Hembua (Vudee) zilifunguliwa katika eneo la Vuasu, na wasichana wakapewa nafasi zaidi shuleni wakisoma pamoja na wavulana.
Mwaka 1954 chama cha siasa cha TANU kilizaliwa na walimu wa Kanisa walihamasishwa kujiunga na vyama vya siasa ili Kanisa lisiachwe nyuma kwenye mageuzi.
Mwaka 1955 chuo cha Lwandai kilihamia Makumira.
Mwaka 1957 Mchungaji D.C Flat alichaguliwa kuwa Mkuu wa Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini na Mchungaji Stefano R. Moshi kuwa Msaidizi wake. Pia eneo la Vuasu lilipata wachungaji wapya wa kihistoria waliomaliza masomo yao Makumira ambao ni Aminieli Kisaka (Kifula) akitokea Mcheni, Paulo Shaidi (Vudee) na Walter Mrisha.
Mwaka 1958 mabadiliko ya uongozi yalifanyika na Mchungaji Stefano Reubeni Moshi aliteuliwa kuwa Rais wa Kanisa la Tanganyika ya Kaskazini akisaidiwa na Mchungaji D.C Flat.
Mwaka 1959 Moses Tezura Mshana alimaliza masomo yake Makumira na kubarikiwa kuwa Mchungaji. Mchungaji Moses Tezura kwa muda mrefu alikuwa mhariri gazeti la Uhuru na Amani lililochapishwa na Kanisa la Kilutheri Tanganyika ya Kaskazini. Mpaka kufikia mwaka huu wa 1959 eneo la Vuasu lilikuwa na sharika tisa zikiwa na jumla ya wakristo 23,000, kama ifuatavyo: Shughatini (3,838), Usangi (3,510), Kifula 3,992), Vudee (2,266), Mbaga (2,541), Bombo (3,206), Mtii (1,860), Ivuga (1,226), na Same (661).
KANISA NA UIMBAJI
Tangu Injili ianze kuhubiriwa katika eneo la Vuasu Julai, 1900, uimbaji umekuwa sehemu kubwa ya ibada ya Kikristo. Na kila wakati Wakristo wamejitahidi kutunga nyimbo zinazopatana na watu wa wakati wao. Nakala ya kwanza ya kitabu cha nyimbo kwa lugha ya Chasu ilitolewa kabla ya mwaka 1912. Nakala hiyo iliitwa “MAIMBO” na ilikuwa na nyimbo 20 tu.
Baada ya hapo nyimbo zilizidi kuongezwa kidogo kidogo mpaka mwaka 1928 pakatokea toleo la pili lililoitwa “Kitabu cha Maimbo.” Toleo hili lilikuwa na Liturgia za majira yote na nyimbo 182 ambazo ziliwaunga Wapare wote toka Kaskazini hata Kusini. Baada ya hapo Kanisa likazidi kuona utajiri wake katika kuimba, na hivyo mwaka 1964 ndipo pakatokea toleo la tatu. Toleo hili likaitwa “Ngazo ya Mrungu” Lenye nyimbo 434, Liturgia pamoja na Katekisimo Ndogo ya Martin Luther.
Nyakati zetu hizi imeonekena kwamba ni muhimu kuendelea kutunza na kutumia Kitabu hiki cha lugha ya Kipare ambacho ni urithi muhimu wa Kanisa la Mungu hapa Upare. Hivyo toleo la tano la kitabu cha Ngazo ya Mrungu limetoka mwaka 2021 kwa ushirikiano wa Dayosisi ya Pare na Dayosisi ya Mwanga. Maboresho mbalimbali yamefanyika katika toleo hili kama vile aya ya siku, sala maalumu kwa majira yote ya mwaka wa kanisa, kuingiza kazini watumishi wa kanisa, kubariki, na kuweka wakfu vifaa mbali mbali vya kanisa.
Hata hivyo nyakati za sasa Uimbaji katika Kanisa hapa Upare umekua sana na hata kutumia utaalam wa kisasa na mchanganyiko wa ala za kimuziki zilizotengenezwa kwa Teknolojia ya hali ya juu. Roho Mtakatifu amekuwa mwalimu bora kuliongoza Kanisa lake tangu mwanzo mpaka sasa ili libaki kuwa Kanisa liimbalo.
MATUKIO YA KIHISTORIA YA KANISA LA TANGANYIKA YA KASKAZINI-ENEO LA VUASU
Mpaka kufikia mwaka 1960 kulikuwa na ongezeko kubwa la sharika katika eneo la Vuasu. Wachungaji na Wainjilisti wenyeji tayari walikuwepo katika sharika za Kifula, Shighatini, Usangi, Same, Mbaga, Bombo, Vudee, Mtii, Chome, Mruma na Ivuga. Ndipo tarehe 02– 07/12/1960 ulipofanyika Mkutano Mkuu wa Kanisa la Tanganyika ya Kaskazini katika Usharika wa Kifula ukiongozwa na neno kuu la Mkutano kutoka 1 Sam.7:12 “Hata sasa BWANA ametusaidia”. Katika Mkutano Mkuu huo ulioongozwa na Raisi wa Kanisa la Kilutheri la Tanganyika ya Kaskazini (Mchungaji Stephano R. Moshi) walifikia uamuzi wa kutumia uongozi wa Kiaskofu katika Kanisa. Sababu kubwa tatu za kufikia uamuzi wa kutumia jina Askofu zilikuwa:
Sababu ya kwanza, Jina Askofu lilitumiwa na vyama vingi vya kimisioni vilivyotuma wamisionari kuja Tanganyika.
Sababu ya pili, neno Askofu lilitumika katika tafsiri za Agano Jipya kwa hiyo watu wengi walielewa vizuri maana yake.
Sababu ya tatu ni kwamba neno Askofu linatumika mara nyingi katika maungamo ya Kilutheri.
Mwaka 1962 sharika mpya za Ntenga, Mhezi na Kilevo zilizaliwa na mwaka huo huo wanafunzi wanne wa uchungaji walibarikiwa kuwa wachungaji, ambao ni Fanuel Solomoni (Mruma), Eduward Mbaruku (Shighatini), Mathias Gerson Mndeme (Mbaga) na Seth Gureni Mnzava (Vudee).
Kwenye Mkutano Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Tanganyika uliofanyika mjini Dar es Salaam tarehe 16–21/06/1963, ilipatanwa pawe na Kanisa moja la Kilutheri. Wajumbe wa Mkutano Mkuu waliweka saini kwenye patano hilo na Kanisa likaanza rasmi tarehe 19/06/1963, nalo likajulikana kama Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini akachaguliwa kuwa Mkuu wa kwanza wa Kanisa.
Kwa kuthamini siku hii tangu wakati huo hata sasa kila tarehe 19 ya mwezi wa Juni au Jumapili inayokaribia tarehe hii tunaadhimisha sikukuu ya KKKT. Sikuhii huadhimishwa na Wakristo wa Dayosisi zote kwa kutoa sadaka maalumu ijulikanayo kama sadaka ya KKKT. Mara baada ya Muungano huu Kanisa la Tanganyika ya Kaskazini lilijulikana rasmi kama Dayosisi ya Kaskazini ambapo eneo lote la Vuasu lilikuwa jimbo la Pare la Dayosisi ya Kaskazini.
Tarehe 13/03/1964 Mchungaji Silas Msangi alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Machame, pia katika mwaka huo Mchungaji Paulo Shaidi alichaguliwa kuwa Mkuu wa Jimbo la Pare.
Mwaka 1965 wanafunzi wawili wa uchungaji walibarikiwa kuwa wachungaji ambao ni Ernesti Mhando (Shighatini) na Nakaza Kabora (Bombo).
Mwaka 1966 kitabu cha Agano Jipya kwa lugha ya Chasu (Kiaghano Kishaa) kilichapishwa ikiwa ni utambulisho wa Wapare (Vaasu). Mwaka huo huo wanafunzi wawili wa uchungaji walibarikiwa kuwa wachungaji ambao ni Stefano Ombeni Msangi (Mbaga) na Elisamia Yoaza Mkaria (Kifula).
Mwaka 1971 shule nyingi za Kanisa zilitaifishwa na walimu wakakabidhiwa serikalini Wizara ya Elimu. Kanisa lilibaki na jukumu la kufundisha dini mashuleni, jukumu linaloendelea kufanyika mpaka sasa katika shule zote nchini.
HISTORIA YA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA
DAYOSISI YA PARE
Mwaka 1967 kwenye Mkutano wa Jimbo la Pare uliokutana usharika wa Mtii wazo la Jimbo la Pare kuwa Dayosisi/Sinodi lilianzishwa; na mwaka huo usharika wa Msangeni ulizaliwa.
Mwaka 1968 Mchungaji Fanueli Solomoni alichaguliwa kuwa Mkuu wa jimbo la Pare na Mchungaji Matiasi Gerson Mndeme kuwa Msaidizi wake; wazo la Jimbo la Pare kuwa Dayosisi/Sinodi liliendelea.
Tarehe 16/10/1969 wazo la Jimbo la Pare kuwa Dayosisi/Sinodi lilifikishwa kwa Askofu Stephano Reuben Moshi na kujadiliwa katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya jimbo iliyokutana usharika wa Same. Katika mwaka huo usharika wa Maore ulizaliwa.
Tarehe 22/01/1970 Mkutano Mkuu wa Jimbo la Pare wa dharura ulikutana usharika wa Same kuzungumzia wazo lao la Jimbo la Pare kuwa Dayosisi/Sinodi. Katika mwaka huo mwanafunzi wa uchungaji Wilsoni Gabrieli Makame (Chome) alibarikiwa kuwa Mchungaji na mwaka huo huo usharika wa Makanya ulizaliwa.
Mwaka 1972 kwenye Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania uliofanyika Bukoba uliridhia Jimbo la Pare liwe Dayosisi. Kutokana na hitaji hilo tarehe 08 – 10/11/1972 katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Pare iliundwa Kamati ya Katiba na kuanza wajibu wake mara moja.
Mwaka 1973 Kamati ilikabidhi katiba kwa Mkutano Mkuu Jimbo la Pare. Mkutano Mkuu uliunda majimbo manne ambayo ni: Jimbo la Kaskazini, Jimbo la Kati, Jimbo la Kusini Mashariki na Jimbo la Kusini Magharibi.
Mwaka 1974 Chediel Emmanuel alibarikiwa kuwa Mchungaji.
Tarehe 20-22/10/1974 Mkutano Mkuu wa Jimbo la Pare ulikutana Kifula, na kuchagua viongozi wa itakayokuwa Dayosisi ya Pare. Mkutano huo ukawachagua Mchungaji Eliewaha Elia Mshana kuwa Askofu wa kwanza na Mchungaji Stefano Ombeni Msangi kuwa Msaidizi wa Askofu.
Mwaka huo wa 1974 Mikutano Mikuu ya majimbo ikafanya uchaguzi wa wakuu wa majimbo na wasaidizi wao.
- Jimbo la Kaskazini Mkuu wa Jimbo wa kwanza alikuwa Mchungaji Elisamia Mkaria na Mchungaji Mbazi Marisa akawa makamu Mkuu wa Jimbo.
- Jimbo la Kati Mkuu wa Jimbo wa kwanza alikuwa ni Mchungaji Wilsoni Gabrieli Makame na Mchungaji Samweli Malaki akawa makamu Mkuu wa Jimbo.
- Jimbo la Kusini Mashariki Mkuu wa Jimbo wa kwanza alikuwa ni Mchungaji Nakaza Kabora na Mchungaji Ezekieli Senkoro akawa makamu Mkuu wa Jimbo.
- Jimbo la Kusini Magharibi Mkuu wa Jimbo wa kwanza alikuwa ni Mchungaji Paulo Shaidi na Mchungaji Paulo Mtae akawa makamu Mkuu wa Jimbo.
Wakristo wa Jimbo la Pare wakiwa na hamu na furaha ya kuwa na Dayosisi yao walionyesha moyo kwa kutoa mali na fedha zao. Michango iliyochangwa na wakristo kwa ajili ya kuanzisha Dayosisi hii ilifikia shilingi laki tano hamsini na tatu elfu mia nane thelethini na saba na senti sabini na tano (Shs. 553,837.75). Katika mwaka huo Mchungaji Martini Shafuri aliitwa Mbinguni.
Mwaka 1975 Maofisa na Wakuu wa Idara mbalimbali waliteuliwa. Katibu Mkuu wa kwanza akawa Bwana Abraham Shaidi, Msaidizi wa Katibu mkuu akiwa ni bwana Davis Irigo, Mtunza hazina akawa bwana Amanieli Mzanyuma, Idara ya Vijana akawa Mchungaji Seth Gureni Mnzava, Idara ya Elimu ya Kikristo akawa Mchungaji Fanueli Solomoni, Idara ya wanawake akawa Bi Foibe Mndeme, Mwandishi akawa bwana Gabrieli Mgonja, Dereva akiwa ni bwana Gadieli Mjema, na mhudumu wa Ofisi akiwa ni bwana Hagai Mnango.
Tarehe 16/03/1975 Dayosisi ya Pare ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ilizinduliwa rasmi na kusimikwa viongozi wake. Mpaka mwaka wa kuzindua Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare, kazi ya Mungu ilikuwa imeendelea kwa kiasi kikubwa kwani tayari kulikuwa na sharika kumi na sita (16).Hata hivyo wachungaji wenyeji watatu (3) waliitwa mbinguni nao ni: Mchungaji Yonazi Kikuji (Ntenga), Mchungaji Silas F. Msangi (1964, Kifula), na Mchungaji Martini Shafuri (1974, Mbaga).
UONGOZI WA KANISA LA KIINJILI LA KILUTHERI TANZANIA
DAYOSISI YA PARE
Tangu kuanzishwa kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare kumekuwa na awamu tatu za uongozi. Awamu ya kwanza iliongozwa na Askofu Eliewaha Elia Mshana (1975 mpaka 1994). Awamu hii kazi ya Injili iliendelea kwa nguvu, idadi ya Sharika zikiongezeka na Wachungaji kuongezeka. Kihistoria ni wakati wa uongozi wake tendo la Watheolojia Wanawake kubarikiwa kuwa wachungaji lilikubaliwa. Mwaka 1992 Watheolojia wanawake watatu, Sara Mwanga (Shighatini), Esther Ngumuo (Kifula) na Joyce Karata (Shighatini) walibarikiwa.
Askofu Dkt. Eliewaha Elia Mshana alistaafu rasmi mwaka 1994 baada ya kuitumikia Dayosisi ya Pare kwa miaka 20.
Aliyekuwa msaidizi wa Askofu wa kwanza Mchungaji Stefano Ombeni Msangi akachaguliwa kuwa Askofu wa pili wa Dayosisi ya Pare mwaka 1994. Mchungaji Stefano Ombeni Msangi aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa pili wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare, katika ibada iliyoongozwa na Baba Askofu wa kwanza wa KKKT Dayosisi ya Pare mwaka 1995 ibada iliyofanyika Usharika wa Same.
Awamu hii kulikuwa na msukumo mkubwa katika upande wa Kaskazini wa eneo la Dayosisi ya Pare wa kuhitaji kuwa na Dayosisi mpya ya Mwanga. Kazi ya Injili iliendelea na sharika ziliongezeka na idadi ya Wachungaji kuongezeka na kuwa na kozi maalumu ya Wachungaji katika chuo cha Mafunzo na Uongozi Usangi, kubuni miradi kadhaa ya uchumi na maendeleo, elimu pamoja na afya.
Katika Sinodi/Mkutano Mkuu wa 14 uliofanyika shule ya Viziwi Mwanga tarehe 30/11-01/12/2008Askofu Stephano Ombeni Msangi alimaliza muda wake wa uongozi akiwa ameitumikia Dayosisi kwa miaka 14. Katika kipindi chake cha uongozi alihudumu pamoja na wasaidizi wa Askofu wafuatao; Mchungaji Aminieli Sauli Ndoveni, Mchungaji Samweli Malaki na Mchungaji Eliraha Mmwiri.
Mchungaji Dr Leonard Mtaita (aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCT) alichaguliwa kuwa Askofu mteule wa Dayosisi ya Pare akiwa nje ya nchi lakini aliushukuru Mkutano Mkuu kwa kumchagua na kutoa udhuru wa kupokea wajibu huo.
Kwa kufuata Katiba ya Dayosisi ya Pare, Halmashauri Kuu ilimpa wajibu Mchungaji Eliraha Mmwiri aliyekuwa Msaidizi wa Askofu wa wakati huo kuongoza Dayosisi katika kipindi cha mpito.
Halmashauri Kuu ya Kanisa ilimpa wajibu Askofu Dkt. Stephen Munga wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki kufanya majukumu ya Kiuaskofu na maridhiano ya washarika wa upande wa kaskazini wa Dayosisi ya Pare wakati Dayosisi inapojiandaa kwa Mkutano Mkuu maalumu wa uchaguzi wa viongozi wapya. Tarehe 11/10/2009 ibada maalumu ya maridhiano ilifanyika Shighatini ikiongozwa na Mkuu wa Kanisa wa Wakati huo Askofu Dkt Samson Mushemba.
Tarehe 02-04/05/2010 kwenye Sinodi/Mkutano Mkuu wa 15 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare, uliofanyikia usharika wa Same, ulimchagua Mchungaji Charles Rabsoni Mzanyuma Mjema kuwa Askofu Mteule wa Dayosisi ya Pare ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, na Mchungaji Timothy Jonas Aseri Msangi alichaguliwa kuwa Msaidizi wa Askofu mteule.
Tarehe 10/10/2010 Mchungaji Charles Rabsoni Mzanyuma Mjema aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa tatu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Pare, na kuingizwa kazini kwenye ibada iliyofanyika usharika wa Same. Katika ibada hiyo Askofu Charles Rabsoni Mzanyuma Mjema alimuingiza kazini Mchungaji Timothy Jonas Aseri Msangi kuwa Msaidizi wa Askofu.
Katika awamu hii ya tatu ya Uongozi mambo mengi yamefanyika ikiwa ni pamoja na mabadiliko na maboresho ya mifumo ya kiutendaji na utawala.